Mada:
Ufugaji bora wa kuku
1. Aina za kuku wanaopatika hapa
nchini Tanzania (koo za kuku), elezea aina za kuku wa kienyeji na kisasa
Kuna aina nyingi za kuku
wanaopatikana hapa nchini. Kuku hawa hutambulika kutokana na maumbile yao,
muonekanao na asili wanapotoka.
Kuku
wa Asili
·
Kuchi
– Wana miili mikubwa, miguu mirefu na ukiko wenye umbile la uaridi (rose)
·
Kishingo
– Ni kuku wasio na manyoya shingoni na hii ndio asili ya jina lake. Wana miguu
ya urefu wa wastani na miili ya ukubwa wa wastani
·
Tewe
– Wana miguu mifupi na maumbile madogo, ni watagaji na waatamiaji wazuri
·
Bukini
– Ni aina ya kuku wasio na manyoya marefu mikiani
·
Kinyafu
(Njanjame) – Wana manyoya yaliyokunjamana na maumbile ya aina tofauti
Kuku wa kisasa
Hawa wamegawanyika katika makundi
makuu mawili:- Kuku wa Nyama na kuku
wa Mayai
Kuku wa Nyama – Ni
maarufu sana kwa ukuaji wao wa haraka na uzalishaji wa nyama kwa wingi
·
White Cornish (Ni weupe na
hupatikana kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini)
·
White Plymouth Rock (Nao ni weupe
na michirizi myeusi)
Kuku wa Mayai – Ni
maarufu kwa utagaji wao wa mayai kwa wingi
·
White leghorn – Ni weupe na
hutaga mayai mengi, wana maumbo madogo na hivyo huhitaji chakula kidogo
·
Rhode Island Red – Wana rangi
nyekundu, kutokana na maumbo yao kuwa makubwa, wafugaji huwatumia pia kwa
uzalishaji wa nyama
·
New Hampshire – Wana rangi ya
kahawia (Brown) nao wana maumbo makubwa ni watagaji wazuri lakini pia
wazalishaji wa nyama
2. Taratibu za kupokea vifaranga, au
kuku wakubwa kutoka kwa mzalishaji wa vifaranga, au sokoni wanapouzwa.
Siku zote mfugaji anashauriwa
kutafuta vifaranga au kuku wakubwa kutoka kwa wazalishaji waaminifu ambao
huzingatia kanuni za ufugaji bora ikiwepo kuzingatia ratiba zote za chanjo ili
kuzuia hasara inayoweza kujitokeza kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Kabla ya kupokea vifaranga
mfugaji anashauriwa kufanya maandalizi muhimu ikiwepo kuandaa banda au chumba
cha kulelea vifaranga, ikiwemo kuhakikisha kuwa ameandaa vyombo vya chakula na
maji, ameandaa chakula kwa ajili ya vifaranga, kuhakikisha kuwa joto la chumba
atakacho wafugia ni la wastani kulingana na umri wao.
3. Uleaji wa vifaranga elezea:
njia ya kubuni na njia ya asili kama zipo.
Zipo njia tofauti za kulea
vifaranga. Vifaranga huweza kuachwa na mama yao ili awalee au kulelewa kwa
kutumia nishati. Mahitaji makubwa ya vifaranga kutoka kwa mama yao ni joto,
hivyo mfugaji anaweza kuwalea vifaranga kwa kuwapatia joto kutokana na vyanzo
mbalimbali kama vile taa ya chemli au jiko la mkaa. Lakini pia vifaranga huweza
kulelelewa bila nishati kwa kutumia chumba kisichopitisha upepo wala baridi
wakati wa mchana na kuwaweka katika boksi au kasha lilitandazwa maranda ya mbao
au matambara wakati wa usiku, katika utaratibu huu, vifaranga watapeana joto
wao kwa wao.
4. Sifa za kuku bora.
Sifa za kuku bora hutofautiana
kulingana na malengo ya mfugaji. Ikiwa ni kwa lengo la nyama basi aweze
kuzalisha nyama kwa wingi na kama ni kwa lengo la mayai basi aweze kutaga mayai
mengi. Kwa ujumla kuku bora anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
Sifa za Jogoo bora
·
Mwili mkubwa
·
Wanaokua haraka
·
Wenye bidii ya kupanda
·
Uwezo wa kuitia matetea chakula
·
Asiwe mkali kwa vifaranga
Sifa za tetea bora
·
Mwenye mwili mkubwa
·
Wanaokua haraka
·
Wanaotaga mayai mengi na makubwa
·
Uwezo mzuri wa kuatamia na
kutotoa mayai mengi
·
Uwezo mzuri wa kulea vifaranga
Mada: Mifumo ya ufugaji kuku,
Utofauti
wa ufuganji wa bandani, huria na nusu huria
Ipo
mifumo tofauti ya kufuga kuku
Mambo
yanayomfanya mfugaji aamuue aina ya mfumo wa kutumia katika ufugaji wake ni
uwezo wake kifedha na ukubwa wa eneo lake la kufugia.
Mfumo huria
Kuku
huachwa nje wajitafutie chakula na maji wao wenyewe. Mfumo huu hutumiwa zaidi
na wafugaji wa kuku wa asili. Ni mara chache sana kuku kupewa chakula cha ziada
na mahali pa kulala katika mfumo huu.
Faida za mfumo huria.
·
Ni mfumo rahisi ka mfugaji kwa
sababu kuku hujihudumia kwa sehemu kubwa
·
Ni mfumo wenye gaharama ndogo kwa
sababu hakuna gharama ya kuwapa chakula wala kuwajengea sehemu ya kulala.
·
Ni mfumo unaowawezesha kuku
kupata mazoezi ya kutosha
·
Ni mfumo unaowafanya kuku
kujipatia virutubisho mchanganyiko katika mazingira jambo ambalo ni zuri
kiafya.
Hasara za mfumo huria
·
Kuku huwa hatarini kuibiwa,
kukanyagwa na magari, kudhurika na hali mbaya ya hewa na wanyama wakali kama
vicheche, mwewe nk.
·
Vifaranga wengi hufa na kupotea.
·
Kuku huharibu mimea ya bustanini
na mazao mengine na hivyo huweza kusababisha ugomvi na majirani.
·
Kuku hutaga sehemu yoyote na
upotevu wa mayai ni mkubwa.
·
Ni vigumu kufuatilia afya ya kuku
kwa karibu na hivyo ni vigumu kutoa tiba na kinga kwa wakati.
·
Ni vigumu kutunza kumbukumbu
sahihi za ufugaji.
·
Ni rahisi kuku kuambukizwa
magonjwa na kuku wengine.
Mfumo wa nusu huria
Katika
mfumo huu, kuku hufugwa kwenye banda lililozungushiwa uzio ili kuwazuia kuku
wasiende mbali. Kuku huwa na uhuru wa kukaa aidha ndani ya banda au nje ya
banda kwenye eneo lililozungushiwa uzio.
Faida za mfumo wa
nusu huria
·
Kuku huwa salama dhidi ya maadui
na hali mbaya ya hewa.
·
Mfugaji huweza kuwapatia kuku
wake virutubisho muhimu na matokeo yake ni ongezeko la uzalishaji.
·
Ni rahisi kudhibiti wadudu na
vimelea vinavyosababisha magonjwa kwa kuku.
·
Ni rahisi kuwatenganisha kuku
katika makundi tofauti na kuwahudumia ipasavyo.
·
Ni rahisi kutambua kuku wagonjwa
na kuwatibu mapema.
·
Kuku hupata mwanga wa jua wa
kutosha pamoja na hewa safi na wakati wa jua kali wanaweza kuingia ndani ya
banda na kukaa kivulini.
·
Kuku hudhibitiwa wasiharibu mazao
na hivyo kuzuia ugomvi na majirani.
·
Upotevu wa kuku na mayai hupungua
kwa kiasi kikubwa.
·
Ni rahisi kukusanya na kutumia
mbolea ya kuku kwa ajili ya matumizi ya bustani.
·
Ni rahisi kutunza kumbukumbu za
ufugaji
·
Ni mfumo mzuri kwa wafugaji wasio
na maeneo ya kutosha hasa wafugaji wa mijini
Hasara za mfumo wa
nusu huria.
·
Mfugaji atahitaji muda wa ziada
kwa ajili ya kuwahudumia kuku kama kuwapa chakula na maji
·
Mfugaji atahitajika kuwatafutia
kuku virutubisho vyote muhimu.
·
Linahitajika eneo kubwa kiasi la
kufugia.
·
Kuna gharama ya ziada ya
kutengeneza banda na wigo na ya kununua au kutengeneza chakula cha kuku.
Mfumo wa ndani ya
banda
Kwenye mfumo huu kuku hukaa ndani
banda muda wote. Ni mfumo unaotumiwa zaidi na wafugaji wa kuku wa kisasa hasa
katika maeneo ya mijini.
Faida za mfumo wa
ndani ya banda.
·
Ni rahisi kutambua na kudhibiti
magonjwa
·
Ni rahisi kudhibiti upotevu wa
kuku, mayai na vifaranga
·
Ni rahisi kuwapatia chakula
kulingana na mahitaji yao kwa kila kundi
·
Ni rahisi kuwatambua na kuwaondoa
kuku wasiozalisha katika kundi
Changamoto za
kufugia ndani ya banda tu
·
Unahitajika muda wa kutosha
kuwahudumia kuku
·
Ni mfumo unaoambatana na gharama
za kujenga banda na kuwanunulia kuku chakula.
·
Ugonjwa ukiingia ni rahisi kuku kuambukizana.
Ujenzi wa banda
bora la kuku
v Sifa ya banda bora la kuku
·
Liwe imara kuzuia maadui kama panya,
vicheche, paka, nyoka na wezi.
·
Liwe na uwezo wa kupitisha hewa
na mwanga wa kutosha.
·
Liwe na paa refu na mlango mpana
wa kuruhusu mtu mzima kuingia kufanya usafi na kutoa huduma nyingine katika
banda kwa uhuru.
·
Kuta na sakafu visiribwe kusiwe
na nyufa ili kuondoa maficho ya wadudu kama papasi, viroboto, utitiri n.k.
·
Liwe na ukubwa wa kutosha idadi
ya kuku waliopo.
·
Paa liwe imara na lisivuje. Vifaa
kama mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. vinafaa kutumika kuezeka. Lijengwe
mahali pasipotuamisha maji.
·
Lijengwe uelekeo wa
Mashariki-Magharibi ili kuzuia mwanga wa jua jua kuingia bandani
Mada: Magonjwa na wadudu wanaoshambulia kuku na jinsi
ya kukinga.
- Magonjwa ya kuku husababishwa na nini?
Zipo
sababu mbalimbali zinazosababisha magonjwa kwa kuku.
·
Magonjwa yanayosababishwa na
vimelea vya Bakteria
·
Magonjwa yanayosababishwa na
virusi
·
Magonjwa yanayosababishwa na
wadudu wa nje ya ngozi
·
Magonjwa yanayosababishwa na
minyoo
·
Magonjwa yanayosababishwa na
vimelea jamii ya protozoa
·
Magonjwa yanayosababishwa na
fangasi na
·
Magonjwa yanayosababishwa na
lishe duni
- Taja Magonjwa yanayoshambulia kuku?
Magonjwa
yanayoshambulia kuku ni mengi na baadhi ni kama yafuatayo
Magonjwa
yanayosababishwa na bakteria
- Taifodi ya kuku (Fowl typhoid)
- Kuharisha kinyesi cheupe (Bacillary white diarrhea)
- Kipindupindu cha kuku (Fowl cholera)
- Mafua ya kuku (Infectious corryza)
- Kolibasilosis (Colibacillosis)
Magonjwa
yanayosababishwa na virusi
- Mdondo/Kideri/Lufuo (Newcastle Disease)
- Gumboro (Infectious Bursal Disease)
- Mareksi (Marek’s Disease)
- Ndui ya kuku (Fowl pox)
Magonjwa
yanayosababishwa na Protozoa
Ugonjwa
wa kuhara damu (Coccidiosis)
- Taja Wadudu wanaoshambulia kuku?
·
Kupe
·
Papasi
·
Utitiri
- Elezea dalili kila ugonjwa?
Dalili
za magonjwa ni nyingi na si rahisi kuzielezea kwa kila ugonjwa ila kwa ujumla
kuku mgonjwa huonesha dalili zifuatazo:
·
Huonekana mchovu na dhaifu
·
Hula/kunywa kidogo au zaidi ya
kawaida
·
Hutoa kamasi puani, ute na
matongotongo
·
Huwa na manyoya yaliyo vurugika
·
Hupumua kwa shida au kwa sauti
·
Sehemu ya kutolea haja kubwa huwa
na unyevunyevu na wakati mwingine kinyesi hugandia
·
Huharisha na wakati mwingine
hutoa kinyesi chenye damu au minyoo
·
Hutaga mayai machache au husimama
kutaga kabisa
·
Hujitenga na wenzao katika kundi
·
Husinzia muda wote
- Athari za magonjwa?
·
Husababisha kuku kukua taratibu
·
Kuku hupunguza uzalishaji
·
Huwafanya kuku kuwa wadhaifu
·
Husababisha vifo kwa kuku
·
Husabisha hasara kwa mfugaji
- Kinga na tiba?
·
Magonjwa ya kuku huweza kukingwa
na mengine huweza kutibiwa
·
Kinga
·
Zingatia usafi wa banda na vyombo
vya kulia chakula
·
Hakikisha banda linakuwa kavu
muda wote
·
Banda liwe na hewa na mwanga wa
kutosha
·
Kuku wagonjwa watengwe na kuku
wazima
·
Kuwe na dawa ya kunawa miguu ili
kuua vijidudu mlangoni (Footbath)
·
Kuku wageni wasichanganywe na
kuku waliopo hadi baada ya wiki mbili
·
Kuku wapewe chanjo za kuzuia
magonjwa mbalimbali na ratiba ya chanjo izingatiwe
- Tiba za asili kama zipo.
Zipo
dawa za aina mbalimbali za asili zinazopatikana kwenye mazingira ya vijijini
ambazo zinaweza kutibu baadhi ya magonjwa ya kuku. Baadhi ya dawa hizo ni kama
zifuatazo:-
Shubiri mwitu (Aloe
vera)
Hutumika
kutibu magonjwa mbalimbali ya kuku.
Kutibu
vidonda vinavyotokana na ndui ya kuku au aina nyingine za vidonda
Maandalizi
- Chukua majani ya Shubiri mwitu na kuyachana vipande vidogo vidogo.
- Vitwange na pumba kidogo na kuvianika.
- Vikikauka vitwange na kuchekecha upate unga laini.
- Hifadhi unga katika chombo kisafi na kikavu.
Matumizi
Safisha
vidonda vilivyotokana na ndui au vidonda vyovyote vile na maji safi yaliyo na
chumvi kiasi.
Pakaa
unga wa Shubiri mwitu katika vidonda vilivyosafishwa.
Utapakaa
unga huu kila siku mpaka vidonda vitakapo pona
Shubiri mwitu pia
hutumika kudhibiti magonjwa mengine ya kuku
Maandalizi
- Chukua jani moja la Shubiri mwitu lenye ukubwa wa wastani.
- Likate katika vipande vidogo vidogo.
- Loweka vipande ulivyokata katika maji kiasi cha lita mbili kwa muda wa masaa 12.
Matumizi
Kuku
wapewe maji haya wanywe kila siku (Ni muhimu mfugaji kuhakikisha kuwa hakuna
maji mengine zaidi ya haya yenye dawa)
Dawa
hii inafanya kazi ya kuwakinga kuku dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Badilisha
maji hayo kabla hayajaanza kuchacha na kuwatengenezea dawa nyingine. Hakikisha
chombo kinasafishwa vizuri kabla ya kuwawekea dawa nyingine
Majani ya Mpapai
Hutumika
kutibu magonjwa ya kuharisha kwa kuku
Namna ya kuandaa
- Chukua jani moja bichi la Mpapai na ulipondeponde lilainike kiasi.
- Changanya na maji kiasi cha lita mbili na nusu.
Matumizi kwa kutibu
- Kuku wapewe maji hayo wanywe, wasipewe maji mengine kwa ajili ya kunywa kwa siku angalau nne au zaidi.
- Inafaa zaidi kila siku kuwaandalia dawa mpya ili dawa isiharibike.
Matumizi kama kinga
Hata
kama kuku hawaharishi, wakizoeshwa kunywa maji yenye majani ya mpapai
yaliyopondwa angalau mara tatu kwa wiki watakingwa magonjwa mengi.
Mada: Chakula na
virutubisho vya kuku
·
Virutubisho
vya kuku
Kuku
kama ilivyo kwa wanyama wengine wanahitaji virutubisho ili waweze kuwa na afya
bora. Vyakula vya kuku ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa makundi mbalimbali
kama yafuatayo:-
ü
Vyakula vya wanga (Carbohydrates)
ü
Vyakula vya protini (Proteins)
ü
Vyakula vya mafuta (Fats)
ü
Madini na (Minerals)
ü
Vitamini (Vitamins)
·
Material
ya kutengeneza chakula cha kuku.
Malighafi zinazohitajika katika
kutengeneza vyakula vya kuku ni pamoja na zile zenye mchanganyiko wa makundi ya
virutubisho tulivyotaja hapo juu.
ü
Mahindi yaliyoparazwa/Mtama
ü
Pumba za mahindi/Pumba za mpunga
ü
Mashudu ya alizeti/Mashudu ya
pamba
ü
Madini mchanganyiko
ü
Chumvi ya mezanio
ü
Chokaa ya mifugo/unga wa
mifupa/DCP
ü
Vumbi la dagaa/Dagaa waliosagwa/Damu
iliyokaushwa
ü
Vitamini
·
Ratio
bora inayotakiwa kutegeneza chakula cha kuku
Yapo
makundi mbalimbali ya kuku na kila kundi lina chakula cha aina yake ila kwa
ujumla chakula kifutacho kinafaa kwa kuku wanaotaga na kuku wazazi
Aina ya
vyakula
|
Kiasi
(Kilo)
|
Mahindi yaliyo parazwa
|
8
|
Mtama
|
3.5
|
Pumba ya mahindi
|
3.25
|
Mashudu ya Alizeti
|
5.5
|
Dagaa waliosagwa
|
4
|
Chokaa ya mifugo (Au Unga wa mifupa)
|
0.75
|
Madini mchanganyiko
|
0.05
|
Chumvi ya mezani/jikoni
|
0.05
|
JUMLA
|
25
|
·
Sifa
ya chakula bora cha kuku
Chakula bora cha kuku ni kile
chenye virutubisho muhimu kwa ajili ya kundi husika la kuku, kwa ujumla
kinatakiwa kuwa na mchanganyiko wa Wanga, Protini, Mafuta, Madini na Vitamini.
Aidha kuku wapewe maji ya kunywa ambayo ni safi salama muda wote.
Kutaga na kutamia mayai, Elezea
·
Muda
wa kuku kuanza kutaga au kuliwa nyama.
Kuku huanza kutaga katika umri
tofauti tofauti kulingana na aina ya kuku, kama ni wa kisasa au wa kienyeji.
Kwa kawaida kuku wa kisasa huanza kutaga wakiwa na umri wa wiki 18 hadi 22
lakini kuku wa kienyeji wengi wao huanza kutaga wakiwa na umri wa wiki 24.
Aidha kuku wa nyama wa kisasa huanza kufaa kwa ajili ya nyama wakiwa na umri wa
wiki 7, kuku machotara huweza kufaa kwa ajili ya nyama wakiwa na umri wa miezi
mitatu hadi mine. Kuku wa kienyeji kabisa huanza kufaa kuliwa nyama wakiwa na
umri wa miezi 5 na kendelea.
·
Jinsi
ya kuandaa viota vya kutagia.
Ili kuku aweze kutaga anahitaji
sehemu tulivu na iwekwe kiota cha kutagia. Zipo aina nyi8ngi za viota kulingana
na uwezo wa mfugaji. Mfugaji anawza kutengeneza viota vya mbao, au kukata
boksi, au kukata ndoo na kuvijaza mchanga au kutengeneza viota kwa kutumia
nyasi kavu au majani ya mgomba. Ni muhimu kiota kikaandaliwa wakati kuku
anapoanza kuonesha dalili za kutaka kuanza kutaga. Kiota kinyunyiziwe dawa ya
kudhibiti wadudu au majivu ili kuzuia wadudu wasumbufu kama vile utitiri.
·
Utunzaji
bora wa mayai
Mayai yatunzwe sehemu kavu na
isiyo na joto kali, boksi liliojazwa mchanga safi au kasha la kuhifadhia mayai
linafaa kutumika kwa ajili ya kuhifadhia mayai. Mayai kwa ajili ya kutotolesha
yahifadhiwe kwa kuwekwa katika sehemu ya kuhifadhia kwa kuwekwa sehemu butu iwe
juu (Sehemu butu ni ile yenye hewa) hii itasaidia kiini tete kuendelea kuwa na
uhai. Aidha mayai machafu yasafishwe kwa spiriti ili kusaidia kuua wadudu wa
maradhi. Mayai kwa ajili ya kutotolesha yasizidi siku 14 toka kutagwa, yai
lililokaa muda mrefu hupoteza uwezo wa kutotolewa
Njia za kutotolesha vifaranga
bora, Elezea
Ø Asilia Kutumia kuku kwa ajili ya
kuatamia mayai, kuku waatamiaji wachaguliwe kutoka miongoni mwa kundi na wapewe
mayai yasiyozidi 10 kwa ajili ya kuatamia
Ø TeknolojiaKwa kutumia mashine za
kutotolesha mayai (Incubators)
Ø Ubunifu Kwa kutumia pumba za mahindi
Mbinu za kuku kuatamia mayai
mengi kwa njia, Elezea
Ø Asilia Kuku hana uwezo wa kuatamia mayai
mengi zaidi ya yale aliyoyataga. Inashauriwa kuku awekewe mayai ambayo ana
uwezo wa kuyaatamia na kutotoa vifaranga. Kuku apewe mayai 10 hadi 12 ili aweze
kuyaatamia na yote yaweze kufikiwa na joto.
Ø Teknolojia Zipo teknolojia mbalimbali za
kutotolesha mayai, mojawapo ambayo ni maarufu sana ni kwa kutumia mashine za
kutotolesha mayai. Zipo mashine za kutumia umeme, mafuta ya taa na sola
Ø Ubunifu Wafugaji wengi siku hizi wamebuni
njia mbalimbali za kutotolesha mayai, baadhi yao hutumia pumba za mahindi
kutotolesha mayai. Mayai huwekwa ndani ya pumba na kuachwa kwa muda wa siku 21
kwa ajili ya kutotoleshwa. Njia hizi si za uhakika sana kwani mayai mengi
huharibika
0 comments:
Post a Comment